2 Corinthians 10

Paulo Atetea Huduma Yake

1 aBasi, mimi Paulo ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Al-Masihi, mimi niliye “mwoga” ninapokuwa pamoja nanyi ana kwa ana, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi! 2 bNawaomba nitakapokuja kwenu nisiwe na ujasiri dhidi ya watu fulani, kama ninavyotazamia kwa wale wanaodhani kwamba tunaishi kwa kufuata namna ya ulimwengu huu. 3 cIngawa tunaishi duniani, hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo. 4 dSilaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome, 5 etukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Al-Masihi, 6 ftena tukiwa tayari kuadhibu kila tendo la kutotii, kutii kwenu kutakapokamilika.

7 gAngalieni yale yaliyo machoni penu. Kama mtu yeyote anaamini kuwa yeye ni mali ya Al-Masihi, basi kumbuka kuwa kama ulivyo wa Al-Masihi, vivyo hivyo na sisi ndivyo tulivyo. 8 hBasi hata kama nikijisifu zaidi kidogo kuhusu mamlaka tuliyo nayo, ambayo Bwana alitupa ili kuwajenga wala si kuwabomoa, mimi sitaionea haya. 9 iSitaki nionekane kama ninayejaribu kuwatisha kwa nyaraka zangu. 10 jKwa maana wanasema, “Nyaraka zake ni nzito na zenye nguvu, lakini ana kwa ana ni dhaifu na kuzungumza kwake ni kwa kudharauliwa.” 11 kWatu kama hao wajue ya kuwa, yale tusemayo kwa barua tukiwa hatupo pamoja nanyi, ndivyo tulivyo na ndivyo tutakavyofanya tutakapokuwa pamoja nanyi.

12 lHatuthubutu kujiweka kwenye kundi moja au kujilinganisha na hao wanaojitukuza wenyewe kuwa wao ni wa maana sana. Wanapojipima na kujilinganisha wenyewe kwa wenyewe, wanaonyesha ya kuwa hawana busara. 13 mLakini sisi hatujajivuna kupita kiasi, bali majivuno yetu yatakuwa katika mipaka ile Mungu aliyotuwekea, mipaka ambayo inawafikia hata ninyi. 14 nKwa maana hatukuwa tunavuka mipaka katika kujisifu kwetu, kama vile ambavyo ingekuwa kama hatukuwa tumekuja kwenu. Kwa maana sisi ndio tuliokuwa wa kwanza kuja kwenu na Injili ya Al-Masihi. 15 oWala hatuvuki mipaka kwa kujisifu kwetu kwa ajili ya kazi iliyofanywa na watu wengine. Tumaini letu ni kwamba imani yenu inavyozidi kukua, eneo letu la utendaji miongoni mwenu litapanuka zaidi, 16 pili tuweze kuhubiri Injili sehemu zilizo mbali na maeneo yenu. Kwa maana hatutaki kujisifu kwa ajili ya kazi ambayo imekwisha kufanyika tayari katika eneo la mtu mwingine. 17 qLakini, “Yeye ajisifuye na ajisifu katika Bwana.” 18 rKwa maana si yeye ajisifuye mwenyewe akubaliwaye, bali yeye ambaye Bwana humsifu.
Copyright information for SwhKC